Kamanda wa polisi kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema kuwa jeshi la polisi wamewakamata watuhumiwa sugu 103 wa makosa mbalimbali ya uhalifu ikiwemo unyang’anyi wa kutumia nguvu.

Kamanda Sirro amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni iliyofanyika kwa wiki moja kuanzia Desemba 2 mwaka huu katika maeneo mbalimbali kwa nyakati tofauti.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni kuvunja nyumba usiku na kuiba; wizi kutoka maungoni; kucheza kamari; kubughudhi abiria; wizi wa magari; kutengeneza, kuuza na kunywa pombe haramu ya gongo; na uvutaji bangi.

Sirro amesema operesheni hiyo ni endelevu na kuwaomba raia wema kuendelea kutoa taarifa za uhakika za kuhusu uhalifu unaotendeka, uliotendeka na unaotarajiwa kutendeka.

Wakati huo huo, Sirro alisema Polisi kupitia kikosi chake cha usalama barabarani kimekamata makosa mbalimbali ya usalama barabarani kwa kipindi cha wiki moja kuanzia Desemba 2 kimeiingizia serikali mapato ya ndani ya Sh 451,590,000 katika mkoa wa Dar es Salaam.

Pia amesema idadi ya magari yaliyokamatwa ni 13,496, pikipiki 1,296, daladala 5,713, magari mengine binafsi pamoja na malori 7,783 huku bodaboda waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu na kupakia mishikaki ni wanne.

Vile vile amesema jumla ya makosa hayo yaliyokamatwa yalikuwa ni 15,053 na jumla ya fedha za tozo zilizopatikana ni 451,590,000 na kuwataka madereva kuwa makini katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka ili kuepuka ajali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *