Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema limeweka vikosi maalum maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam ili kuwabaini watu wanaojihusisha na vitendo vya utekaji watu pamoja na uvunjifu wa amani ambavyo vimeleta wasiwasi katika jamii.
Kamishna wa Polisi Kanda hiyo Simon Sirro amesema wameamua kuweka polisi maalum kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kintelejensia katika maeneo mbalimbali.
Maeneo hayo aliyosema Sirro ni sehemu za fukwe za bahari kwa ajili ya kukusanya taarifa na kuzifanyia kazi na kuliweka Jiji la Dar es Salaam salama na kutokomeza vitendo vya kihalifu.
Pamoja na mambo mengine Kamanda Sirro pia amesema kuanzia saa 12 jioni ni marufuku kwa mtoto kukutwa maeneo ya bahari bila uangalizi wa wazazi na kupiga marufuku disco toto ambazo zimekuwa zikisababisha maafa.