Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama amewataka wabunge kutotumia lugha zinazoudhi bungeni kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha kanuni na kukoseana heshima.

Mhagama ambaye anashughulikia Bunge kwa niaba ya Serikali, aliyasema hayo jana bungeni mjini hapa, wakati akitoa taarifa baada ya Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) kudai kuwa serikali imewatumia askari wa usalama barabarani kuingiza mapato huku ikijinadi imeongeza mapato.

Heche alikuwa akichangia mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/2018 uliowasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Philip Mpango.

Akichangia mapendekezo hayo, Heche amesema askari hao wamegeuzwa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) ndogo ya kuongeza mapato na inapongeza polisi kutangaza imekusanya kiasi gani cha fedha.

Heche alisema pia kuwa polisi wa usalama barabarani wamepewa idadi ya makosa matatu ya kukamata kwa siku jambo alilosema ni kugeuza chombo hicho kama sehemu ya mtaji wa mapato.

Mbunge huyo pia alimwambia Dk Mpango kuwa atakuwa wa pili kutumbuliwa (baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, ingawa hakumtaja) huku akimtuhumu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuwa hafanyi vizuri katika kusimamia elimu kwa kuwa wanafunzi wanakosa mikopo na elimu inashuka.

Amesema Profesa Ndalichako alipokuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) alionesha wanafunzi wakiwa wamechora mazombi (vikaragosi) katika karatasi za mitihani, lakini yeye sasa anashindwa kusimamia elimu hasa mikopo kwa wanafunzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *