Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA) imeahidi kuongeza kiwango cha ruzuku kwa Serikali ya Tanzania ili kufadhili miradi ikiwemo kilimo, maji, miundombinu ya barabara na huduma nyingine za jamii ili kuisaidia kufikia maendeleo yaliyokusudiwa kwa wananchi wake.

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Hiroshi (Hiro) Kato alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango jijini Washington D.C nchini Marekani.

Kato alisema Tanzania na Japan ni marafiki wa muda mrefu na kwamba nchi hiyo itaendelea kuisaidia kwa kutekeleza miradi mbalimbali yenye kuleta tija kwa uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania kwa ujumla.

Amesema Japan pia imeamua kuongeza kiwango cha ufadhili kwa Bara la Afrika kutoka Dola milioni 13 ambazo nchi hiyo ilikuwa ikitoa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2013 hadi kufikia dola 30,000 kwa mwaka kuanzia Agosti, 2016 kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Amesema pia kuwa ili kuwajengea uwezo na ujuzi vijana wa Kiafrika, Japan imeanzisha programu ya kutoa elimu ambapo hivi sasa vijana 60 kutoka nchi mbalimbali za Kiafrika wamepelekwa nchini humo kujifunza kwenye vyuo vilivyoko huko na watapelekwa kwenye kampuni na mashamba makubwa yanayojihusisha na kilimo ili wapate uzoefu na kuwa chachu ya mabadiliko watakaporejea katika nchi zao.

Kwa upande wake, Dk Mpango aliishukuru Japan kwa kuisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Ametaja baadhi ya miradi ambayo nchi hiyo inafadhili nchini Tanzania kuwa ni ujenzi wa barabara ya Arusha-Holili hadi Taveta nchini Kenya, ujenzi wa barabara ya Juu (Flyover) ulioanza eneo la Tazara ili kupunguza msongamano jijini Dar es Salaam, miradi ya maji na kilimo cha umwagiliaji.

Ameishukuru pia Serikali ya Japan kwa kufanya utafiti na upembuzi yakinifu wa mradi wa kudhibiti mafuriko ya Mto Kondoa, eneo la mkoa wa Morogoro ili kudhibiti mto huo usiharibu miundombinu ya Reli ya Kati.

Ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kukusanya kodi na kuziba mianya ya upotevu wa fedha za serikali ikiwemo kuanzisha mahakama maalumu ya kushughulika na mafisadi ili kuleta nidhamu katika utumishi wa umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *