Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amewataka viongozi wa serikali na vyama vya siasa kuacha vitendo vya kuingilia mhimili wa Mahakama na kuvunja amri zake.
Jaji Profesa Juma ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wiki ya Sheria inayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao (Februari mosi), siku ambayo ndio itakayoashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka huu 2018.
Wiki ya Sheria itafanyika katika viwanja vya Mahakama vilivyopo mtaa wa Chimala jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli.
Kwa upande mwingine, Jaji Profesa Juma ametoa rai kwa wananchi na wadau wote wa sheria kutembelea Mnazi Mmoja kwa ajili ya kujifunza na kupata huduma mbalimbali za Kisheria kutoka kwa Majaji, Mahakimu, Wasajili, Watendaji, Mawakili wa serikali.
Pia watakuwepo mawakili wanaojitegemea ambao watakuwa tayari kuwasikiliza na kuwahudumia ipasavyo.