Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ametoa siku saba kwa halmashauri zote nchini, kukamilisha mipango ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyo michache, itakayotekelezwa kwa asilimia 100.
Ametoa agizo hilo wakati anafungua kikao kazi cha kujadili Mpango wa Utekelezaji wa Miradi ya Fedha za Maendeleo za Serikali za Mitaa (LGDG) iliyoboreshwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na kushirikisha wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, maofisa mipango, makatibu tawala wasaidizi wa afya.
Amesema serikali inatarajia kutoa Sh bilioni 251 za maendeleo kwa ajili ya serikali za mitaa, kipaumbele cha kwanza kikiwa ni afya iliyotengewa Sh bilioni 69.
Jafo amesema, baada ya kupitia mipango ya halmashauri, imebainika kuwa halmashauri nyingi zimeelekeza fedha hizo kwenye utekelezaji wa miradi midogo isiyo na tija na kwa sasa imekubaliana na Wizara ya Fedha na Mipango kutoa fedha kwa miradi michache yenye tija.
Katibu Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mussa Iyombe aliwataka maofisa mipango, kufanya kazi yao kwa kuzingatia taaluma na kuacha kuwa na nidhamu ya woga katika kuweka mipango katika halmashauri zao.
Mkurugenzi wa Mbulu, Hudson Kamoga aliipongeza serikali kwa kuja na utaratibu huo na kusema utasaidia kuondokana na halmashauri kuwa na miradi viporo.
Mbunge wa Busokelo, Atupele Mwakibete (CCM) aliwataka wabunge, madiwani na wenyeviti wa halmashauri, kuunga mkono pendekezo la serikali la kuwa na miradi michache inayotekelezwa kwa asilimia 100 na kusisitiza kuwa mpango huo utaondoa tatizo la kuwapo kwa miradi viporo iliyokuwa ikitokana na kila diwani kutaka apate mradi.