Ikulu ya White House imesema hakuna ushahidi wowote wa kuashiria kwamba kulikuwa na wizi wa kura katika uchaguzi mkuu wa Marekani uliofanyika tarehe 8 Novemba.
Afisa wa habari wa ikulu Josh Earnest ametupilia mbali madai ya rais huyo mteule kwamba mamilioni ya watu ambao hawakufaa kupiga kura walishiriki katika uchaguzi huo.
Bw Trump alikuwa pia amedai kwamba kulitokea wizi wa kura katika majimbo ya Virginia, New Hampshire na California, majimbo ambayo Hillary Clinton alishinda.
Bw Trump aliyeshinda uchaguzi kwa kupata kura nyingi za wajumbe, alikuwa amelalamika kuhusu uchaguzi huo kupitia Twitter Jumapili.
Kupitia ukurasa wa Twitter Trump aliandika “Ingekuwa rahisi zaidi kwangu kushinda kura za kawaida kuliko Kura za Wajumbe kwa sababu ningehitajika kufanya kampeni katika majimbo 3 au 4 badala ya majimbo 15 ambayo nilitembelea.
Rais huyo mteule alianza kulalamika baada ya maafisa wa kampeni wa Clinton kusema wataunga mkono mchakato wa kuhesabiwa upya kwa kura katika jimbo la Wisconsin ambao ulianzishwa na mgombea wa chama cha Green Party Jill Stein.
Bi Stein pia ameifahamisha bodi ya uchaguzi katika jimbo la Michigan, ambapo ushindi wa Bw Trump wa kura 16 za wajumbe ulithibitishwa Jumatatu, kwamba ataomba kura za urais zihesabiwe upya.
Trump alishinda kwa kura chache zaidi jimbo la Michigan katika kipindi cha miaka 75 na ndiye mgombea wa kwanza wa Republican kushinda katika jimbo hilo tangu 1988.
Juhudi za Bi Stein za kupigania kuhesabiwa upya kwa kura zinasaidiwa na kampeni ya mitandao ya kijamii ya #recount2016 ambao imesaidia kuchangishwa kwa jumla ya $6.3m (£5m).