Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Simon Sirro amewatahadharisha wananchi kote nchini kutokuvuruga uchaguzi wa marudio wa udiwani unaotarajiwa kufanyika kesho.
Sirro amesema kuwa, jeshi lake limejipanga vilivyo kuhakikisha kuwa zoezi hilo la uchaguzi litafanyika kwa amani na utulivu na kwamba ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya uchaguzi ili kuzuia aina yoyote ya uvunjifu wa amani utakaojitokeza.
Kamanda Sirro amesema kuwa “Natoa rai kwa wananchi walioko kwenye maeneo hayo kushiriki zoezi hili la uchaguzi kwa amani na utulivu na wakishapiga kura warejee kwenye maeneo yao na kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa huku wakisubiri kutangazwa kwa matokeo..
Kamanda Sirro vilevile amezungumzia hali ilivyo kwa sasa katika maeneo ya kibiti na Rufiji kuwa hali ni shwari na wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi.