Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amemtaka dereva wa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kulisaidia jeshi hilo katika kukamilisha upelelezi wa shambulio la mbunge huyo.
IGP Sirro amesema kuwa jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Lissu ambaye anapata matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na watu wasiojulikana.
Kamanda Sirro amesema miongoni mwa wanaohitajika kwa kuhojiwa ni dereva wa Lissu ambaye inaelezwa yuko Nairobi anakopatiwa matibabu ya kisaikolojia.
Sirro amesema kuwa “Yule kijana kwenye picha ukimwona yuko vizuri tu, sasa wanaposema anapata huduma ya kisaikolojia wakati kwenye magazeti anaonekana hii inatupa changamoto. Ndugu zangu, mheshimiwa Lissu amepigwa risasi na watu tunaowatafuta, huyo kijana aje. Kuja kwake kutatusaidia kupata majibu ya mambo mengi,”.