Muigizaji wa Marekani, Emma Stone ndiye mwigizaji wa kike anayelipwa pesa nyingi zaidi miongoni mwa waigizaji duniani mwaka huu.
Mwigizaji huyo aliyeigiza katika filamu iliyovuma sana mwaka huu ya La La Land alilipwa $26m (£20m) katika kipindi cha miezi 12 kati ya Juni 2016 na Juni 2017, sana kutokana na ufanizi wa filamu hiyo.
Malipo hayo yalimfanya kuongoza katika orodha ya kila mwaka ya jarida la Forbes, na kuwashinda Jennifer Anniston na Emma Watson.
Jennifer Lawrence, aliyeongoza 2016, alikuwa wa tatu baada ya kulipwa $24m (£19m) mwaka huu.
Mapato ya Emma yalipanda kwa 160% ukilinganisha na mwaka 2016, alipolipwa $10m (£8m).
Mwigizaji huyo wa miaka 28 majuzi alizungumzia mjadala kuhusu pengo la mishahara kati ya waigizaji wa kiume na wa kike, ambapo alifichua kwamba waigizaji wenzake wa kiume wameamua kwa hiari kupunguziwa mishahara ndipo walipwe kiasi sawa.
Jennifer Lawrence alikuwa ameongoza orodha hiyo ya Forbes kwa miaka miwili iliyotangulia, sana kutokana na ufanisi wa filamu za Hunger Games.
Mwaka 2016 alipata $46m (£36m), baada ya kutolewa kwa The Hunger Games: Mockingjay – Sehemu ya Pili 2, makala ya mwisho ya mwendelezo wa filamu hizo.
Mwaka huu, waigizaji wa kike 10 wanaolipwa pesa nyingi zaidi kwa pamoja walipata $172.5m (£134m), kabla ya kutozwa ada na ushuru.