Hosteli mpya za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zilizokuwa zikijengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) zipo katika hatua ya mwisho kabisa za kumalizia ujenzi wake na zinatarajia kuanza kutumika wiki ijayo.
Mabweni hayo yalijengwa kufuati ombi lililotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Rwekaza Mukandala kwa Rais Magufuli katika sherehe za uwekaji jiwe la msingi ujenzi wa maktaba ya kisasa chuoni hapo Juni 2 mwaka jana.
Jumla ya majengo 20 yenye ghorofa nne kila moja yamejengwa katika eneo hilo la mashariki mwa chuo yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo zaidi ya 3,840 kati ya wanachuo 7,000 wanaolazimika kupanga vyumba vya kuishi mitaani kutokana na kukosa nafasi katika mabweni ya chuo yaliyopo.
TBA imetumia wataalamu na vijana wa kitanzania kwa gharama ya TZS bilioni 10 kukamilisha ujenzi huo ikilinganishwa na endapo ingetumia wakandarasi ambao walitaka kulipwa kati ya shilingi bilioni 50 na bilioni 100.