Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezitaka Hospitali na vituo vya Afya nchini kuhakikisha wagonjwa hawauziwi damu.

Ummy amesema hayo kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuchangia damu ambayo inafanywa na Chama cha wanawake wa Tasnia ya Filamu nchini jijini Dar es salaam.

“Napenda kusisitiza damu haiuzwi na kwa mgonjwa yeyote atakayeuziwa damu kwenye kituo chochote cha afya cha Serikali atoe taarifa  kwenye idara husika na atachukuliwa hatua” amesema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amewataka viongozi wa Hospitali na vituo vya Afya vya Serikali wahakikishe kuwa wanaweka matangazo yanayoelimisha wananchi kuwa damu haiuzwi bali inatolewa bila ya malipo na matangazo yaelekeze wananchi sehemu ya kutoa malalamiko.

Waziri Ummy amewaasa wananchi hasa wanaume kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara ili kuweka akiba ya kutosha katika benki ya damu hatimaye kupunguza uhaba wa damu katika benki ya damu na kuokoa vifo vitokanavyo na ukosefu wa damu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *