Aliyekuwa mgombea urais wa chama cha Democratic, Hillary Clinton ameongoza wingi wa kura zaidi ya milioni mbili dhidi ya Donald Trump wa Republican katika kura za kawaida.

Rais Mteule Trump ameshinda uchaguzi huo wa urais uliofanyika tarehe 8 Novemba kwa wingi wa kura za wajumbe na ataapishwa Januari.

Lakini kura za kawaida zinaendelea kuhesabiwa wiki mbili baadaye na kura za Cook Political Report zinaonesha ana kura 62.2m naye Bi Clinton 64.2m.

Hii ni mara ya tano kwa mgombea kuongoza kwa kura za kawaida lakini akashindwa uchaguzini kwani kura za wajumbe ndizo hutumiwa kuamua mshindi.

Mwaka 2000, mgombea wa Democratic Al Gore aliongoza dhidi ya George W Bush kwa karibu kura 544,000.

Baada ya mvutano wa muda mrefu mahakamani, Mahakama ya Juu mwishowe iliamua mshindi wa urais akawa Bush ushindi katika jimbo la kushindaniwa la Florida.

Mwaka huu Bi Clinton alipata kura nyingi katika majimbo kama vile California lakini Bw Trump alishinda majimbo ya kushindaniwa, na kupata kura nyingi za wajumbe.

Mfumo wa kura za wajumbe humfaa zaidi mgombea ambaye anashinda, hata kama kwa kura chache, katika majimbo mengine dhidi ya yule anayeshinda kwa kura nyingi katika majimbo machache.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *