Aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha Chaumma, Hashim Rungwe ameachiwa kwa dhamana na jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), alishikiliwa kwa siku nne akituhumiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kamanda wa Polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema Rungwe aliachiwa kwa dhamana jana usiku kutokana na siku alizokaa mahabusu kuwa nyingi.

Mambosasa amesema pia wamejiridhisha kuwa hawezi kutoweka hata akiachiwa kwa dhamana.

Mambosasa amesema Rungwe akiwa wakili anatuhumiwa kushiriki kufanya udanganyifu kwa mfanyabiashara kutoka Uturuki, Suleiman Ysian ambaye alikuja nchini kununua korosho tani 15  kutoka kampuni ya Les Tropiques Group Mining Sprl Limited.

Amesema mkataba wa ununuzi wa korosho unaonyesha una gharama ya Dola 72,000 za Marekani sawa na Sh161 milioni ambazo  zitalipwa kupitia akaunti ya benki ya wakili Rungwe.

Kamanda Mambosasa amesema inadaiwa mfanyabiashara huyo ameshalipa takriban Sh75 milioni lakini hakuna mzigo  ulionunuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *