Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Harmonize ameachilia video ya wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la Nitaubeba ambao katika video yake, mchumba‘ke Kajala Masanja ndiye ameuza nyago kama video queen.

Harmonize aliutoa wimbo huo jikoni wiki moja iliyopita ukiwa bila video (audio) na kuwashika wengi kwenye mitandao ya kijamii ambapo mapokezi yake yalikuwa ya aina yake kutokana na weledi wake aliouweka katika mashairi, lakini pia midundo ya aina yake.

Ujumbe mkubwa katika wimbo huo ni asilimia mia kwa mia amejitoa kwa mpenzi wake, Kajala na hilo pia kando na maneno linaweza likaonekana kwenye video kwa njia ya vitendo ambapo wengi walikuwa wanafanya mazoezi ya kungunga ndoa yao ambayo vyanzo vya ndani vinasema itakuwa hivi karibuni.

Harmonize na Kajala kwenye video hiyo ambayo ndiyo inashika chati za juu kwa sasa mitandaoni, wanaashiria jinsi harusi yao itakavyokuwa, hasa ikizingatiwa kwamba baada ya kuvishana pete za uchumba miezi michache iliyopita, wengi wanasubiria harusi yenyewe kwa hamu.

Baada ya kuachilia video hiyo, Harmonize alikimbia kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuachia ujumbe maridhawa akidokeza kwamba huo ni mwanzo tu.

Harmonize anasema kuwa, video hiyo ni ‘dedication’ tosha kwa mpenzi wake, Kajala na aliifanya kwa njia ya kipekee kwa ajili yake –maneno ambayo ukisikiliza ngoma yenyewe utakubaliana nayo moja kwa moja bila kuhitaji uchambuzi wa kina.

Pia Harmonize anafunguka kuwa kila neno na kila tukio katika wimbo huo pamoja na video yake ni ishara tu ya kila kitakachotokea katika siku ya ndovu kumla mwanawe, siku ya kufunga pingu za maisha ambayo wangali bado kuiweka wazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *