Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Harmonize amefuta kesi aliyokuwa amemfungulia Kajala Masanja pamoja na binti yake, Paula kwa tuhuma za kusambaza picha na video zake chafu.
Aprili 20, mwaka huu, mwanamama Kajala ambaye ni staa wa Bongo Movies na mwanawe Paula walitiwa mbaroni kisha kuhojiwa kwa saa kadhaa na Jeshi la Polisi kabla ya kuachiwa kwa dhamana wakidaiwa kusambaza picha za utupu zilizodaiwa kuwa ni za Harmonize.
Harmonize amesema kuwa “Sikia, binafsi nimeshaamua kuwasamehe Kajala na Paula, sitaki tena mambo ya kesi, nimeamua acha maisha mengine yaendelee,’’ alisema Harmo na kuongeza;“Namaanisha nimefuta kabisa kesi niliyokuwa nimewafungulia na sitaki tena kusikia mambo hayo,’’.
Aprili 20, 2021 aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ambaye kwa sasa amehamishiwa jijini Dodoma alithibitisha kukamatwa na kuachiwa kwa wawili hao baada ya kutua nchini wakitokea Dubai.
Kamanda huyo aliyataja makosa waliyotuhumiwa nayo kuwa ni kusambaza picha za utupu mitandaoni zinazodaiwa kuwa za Harmonize na msanii huyo ndiye aliyekuwa amefungua kesi hiyo baada ya kufikisha malalamiko yake Polisi katika Kitengo cha Makosa ya Mtandao.
Kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa, wawili hao walikuwa wanaendelea kuripoti Polisi mpaka hapo jalada la upelelezi wa kesi yao litakapokamilika na kufikishwa mahakamani kwa kuwa kesi za aina hiyo huchukua muda mrefu kuzifanyia uchunguzi.