Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameahidi kuzungumza na mwenzake wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene ili kuhakikisha halmashauri zote nchini zinapanga bajeti ya kununua viuadudu katika kupambana na malaria.
Akizungumza baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Mesa kutembelea kiwanda cha kutengeneza viuadudu, Kibaha mkoani Pwani jana, Ummy alisema hatua ya kuzungumza na Waziri wa Tamisemi ni katika kuhakikisha halmashauri zinunue dawa hiyo kwa lengo la kupambana na ugonjwa wa malaria nchini.
Ameongeza kuwa malaria ni ugonjwa unaosumbua watu wengi na unaifanya serikali kutumia rasilimali fedha nyingi. Alisema takwimu za sasa zinaonesha kuwa takribani Watanzania 14 kati ya 100, wanaugua malaria wakati uwezo ni kutengeneza lita milioni sita kwa mwaka.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dk Samwel Nyantahe alisema kiwanda hicho ni cha kipekee Afrika na kina uwezo wa kuzalisha viuadudu kwa ajili ya soko la ndani, Afrika Mashariki na nchi zingine za Afrika. “Faraja iliyopo ni kuwa wenzetu wa Cuba wako tayari kutusaidia katika masoko mengine kwa ajili ya kuuza bidhaa zetu,” alisema.
Kiwanda hicho kilichofunguliwa mwaka jana, kinatarajia kuanza uzalishaji mwishoni mwa wiki hii, ikiwa ni siku kadhaa tangu kupata mkopo wa Sh bilioni nne zikizotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).