Halmashauri nchini zimetakiwa kuhakikisha zinahuisha mipango mikakati yake kwa kuzingatia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) katika mipango yake ya maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Tamisemi, Jeremia Sendoro wakati wa kufunga warsha ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Amesema kama halmashauri itahusisha mipango mikakati yake kwa kuzingatia malengo hayo kutakuwa na ufanisi mkubwa katika utekelezaji.
Sendoro amesema shabaha ya malengo hayo inahusisha malengo 17 ya maendeleo endelevu yanayolenga kukomesha umaskini, njaa na kuimarisha huduma za afya.
Amesema dhana ya mchakato wa maendeleo endelevu kwa Tanzania ni ushiriki wa nchi katika maandalizi ya malengo kabla ya kuridhiwa likiwa ni jambo muhimu katika kuhakikisha malengo hayo yanakuwa ni sehemu ya kutatua changamoto za malengo kuanzia ngazi ya taifa, mikoa na serikali za mitaa.
Aidha aliwataka watendaji wa halmashauri kuona haja ya namna ya kuanza kutumia vifaa kama simu za mkononi katika upatikanaji wa takwimu sahihi kwa wakati wakati wa kufanya maamuzi.
Amesema katika maeneo kwa nchi zilizoendelea, mapinduzi hayo yamechochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya sayansi na teknolojia katika ukusanyaji na usambazaji wa takwimu mbalimbali.
Amesema pia kila halmashauri itenge bajeti yake ya mahitaji ya kuajiri watumishi na vibali vya ajira vitolewe kwa wakati ili kuimarisha utendaji wa kazi na utoaji wa huduma.