Gwiji wa Reggae nchini Jamaicha, Bunny Wailer ambaye ni Swahiba wa Bob Marley amefariki Dunia.
Mwanamuziki huyo kutoka Kingston, Jamaica, alikuwa mmoja waanzilishi wa bendi ya The Wailers pamoja na rafiki yake wa utotoni, Bob Marley.
Kwa pamoja, walipata umaarufu kimataifa kupitia nyimbo zao za reggae kama vile Simmer Down na Stir It Up, kabla ya Wailer kujiondoa mwaka 1974.
Aliendelea mbele na kushinda tuza tatu za Grammys na kutunukiwa Tuzo ya heshima ya Jamaica 2017.
Kifo chake kilithibitishwa na maneja wake Maxine Stowe, na Waziri wa Utamaduni wa Jamaica, Olivia Grange.
Chanzo cha kifo chake hakijulikani, lakini alikuwa amelazwa hospitali tangu alipougua kiharusi Julai 2020.
Mashabiki wake wamekuwa wakimuomboleza nguli huyo wa muziki wa Reggae, baadhi yao wakimtaja kama shujaa.
Nyota huyo, ambaye jina lake halisi ni Neville O’Riley Livingston, alikuwa mwanachama wa mwisho wa bendi ya The Wailers aliyekuwa hai, baada ya kifo cha Bob Marley mwaka 1981 katokana na saratani, na kuuawa kwa Peter Tosh katika kisa cha wizi wa mabavu mwaka 1987.
Livingston alikulia kijiji cha Nine Miles, ambako alilelewa na baba yake aliyekuwa akiuza mboga.
Ni katika kijiji hicho alipokutana mara ya kwanza na Marley, na wawili hao wakatokea kuwa marafiki wakubwa utotoni, ambapo walitunga muziki wao wa kwanza wakiwa shule ya msingi ya Stepney na shule ya upili.
Kufuatia kifo cha baba yake Marley mwaka 1955, mama yake, Cedella, aliolewa na baba yake Livingston.
Awali wavulana hao walilelewa kama ndugu wa kambo hasa baada ya Cedella na Thaddeus kumzaa binti yao, Pearl.