Godliver Gordian anafanya vizuri kwenye tamthilia ya Jua Kali iliyoandaliwa na Lamata na kubeba visa vya kusisimua huku yeye akicheza nafasi ya mateso kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Kwenye tamthilia hiyo, mwanadada huyo ameonekana kuumizwa na mapenzi kwa kuanzisha mahusiano na baadaye kuachwa huku akishindwa kujipa muda na kuamua kuingia kwenye mahusiano mengine.
Amezika mchumba mmoja ambaye walifikia hatua ya ndoa, alifariki kwa ajali akielekea kanisani kufunga ndoa wakati wanaume wengine wawili waliishia kumvisha pete za uchumba na baadaye kumtelekeza.
Ilipofikia sasa Anna anaonekana kuingia kwenye mahaba na rafiki yake waliyewahi kusoma wote ambaye amemrudisha kwenye furaha baada ya kumpoteza mwanaume ambaye alitaka kumuoa.
Katika mahojiano na gazeti hili, msanii huyo amefunguka mambo mbalimbali huku akitaja kuwa anachokiigiza aliwahi kukipitia japo sio kwa namna anayoigiza kwa kuingia kwenye mahusiano bila kujipa muda.
Anasema aliamini Mungu ndiye alimuonyesha na kuamini ndiye mume sahihi kumbe ni akili yake ilitumika kwa kuamini anazungumza naye kwa njia ya sauti.
Mwanadada huyo amekiri wasanii wanakwenda kwa waganga kusafisha nyota huku akithibitisha kuwa na yeye amefika huko.
Anasema alifuatwa na msanii mwenzake na kumwambia akienda kwa mganga kuna kitu anaweza kupata zaidi.