Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema leo anatarajiwa kuhutubia wananchi wa jimbo lake katika uwanja wa Shule ya Msingi Ngarenaro baada ya kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mtego kwake, kwani inaweza kumjenga kisiasa ama kumharibia kutokana na kile atakachotamka katika mkutano huo wa hadhara.
Lema aliyekaa gerezani kwa zaidi ya miezi minne, aliachiwa kwa dhamana Machi 3 mwaka huu na Jaji Fatuma Maghimbi na wadhamini wawili, waliosaini hati ya dhamana ya thamani ya Sh milioni moja kila mmoja.
Gari la matangazo lilikuwa likipita kila kona ya Jiji la Arusha na kutangaza kuwepo kwa mkutano huo na kuhamasisha wananchi wa Jiji la Arusha, kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano huo bila ya kukosa, kwani mbunge huyo ana ujumbe mzito kwa ajili yao.
Hata hivyo, si Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Gulugwa wala Lema mwenyewe aliyekuwa tayari kueleza ajenda ya mkutano huo, kwani simu zao za kiganjani zilikuwa zikiita bila ya kupokewa.
Hata hivyo, mmoja wa madiwani wa Chadema waliotakiwa kutokosa katika mkutano huo, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake, alisema kuwa mkutano huo unatarajiwa kuanza saa 9 mchana katika shule hiyo ya Ngarenaro.
Diwani huyo alisema lengo la mkutano huo wa hadhara wa Lema ni kutaka kuwashukuru wale wote walioshiriki kwa namna moja ama nyingine kufika gerezani, kumfariji na kumwombea kwa siku zote akiwa mahabusu katika Gereza la Kisongo, nje kidogo ya Jiji la Arusha.