Rais wa Gabon Ali Bongo ameapishwa kwa muhula wa pili wa miaka saba kufuatia uchaguzi uliokumbwa na utata ambapo watu kadhaa waliuawa.
Kuapishwa huku kunafanyika siku tatu baada ya mahakama ya katiba kukataa shinikizo za upinzani za kutaka kura kuhesabiwa tena.
Ali Bongo ambaye babake Omar Bongo alikuwa rais wa Gaboin kwa miongo minne, alishinda uchaguzi huo kwa kura zisizozidi 6000.
Hapo awali upande wa upinzani ulikataa matokeo hayo mpaka kusababisha machafuko katika nchi hiyo na kusababisha watu kadhaa kuuawa.
Upande wa upinzani unaoongozwa na Jean Ping ulipeleka kesi ya kupinga matokeo katika mahakama ya kikatiba mpaka hapo juzi hukumu kutoka na Bongo kutangazwa kashinda kihalali.