Mwanamuziki wa hip hop, G Nako kutoka kundi la Weusi amewataka wasanii na watu wanaohitaji kuwekeza na kufanya biashara ya muziki wasiogope changamoto zilizomo.
G Nako amesema kuwa wadau wa muziki wanatakiwa kukubali fursa na uwezo wao wa kuzikabili changamoto huku akiwakosoa wanaweka changamoto hizo hadharani.
Mwanamuziki huyo amesema kwenye kila kazi kuna changamoto nyingi lakini kuziongelea kwenye vyombo vya habari ni kuwakatisha tamaa wale wachanga wanaotaka kuinuka na kuwazuia kuonesha uwezo wao.
Katika hatua nyingine G Nako amesema muziki anaoufanya ni muziki wa ukombozi hivyo kila mtu huwa anawasilisha mawazo kwa mtindo ambao ana uwezo nao na kusisitiza kuwa ukombozi unadaiwa siyo kuombwa.
Pia ameongeza kuwa kundi lake la Nako 2 Nako bado lipo halijavunjika kama jinsi wengi wanayofikiria na tayari wana nyimbo zisizopungua tano zinasubiri kuachiwa.