Fisi wa Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha wamevamia boma la Wamasai katika kata ya Nainokanoka wilayani humu na kuwala watoto wawili, akiwemo wa miezi tisa na kujeruhi watu wengine kadhaa.
Watoto waliouawa wametajwa kuwa ni Akapuko Ngaruma (4) na mdogo wake Esupati Ngaruma aliyekuwa na miezi tisa tu.
Diwani wa Kata ya Nainokanoka, Edward Maura, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro, amethibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa kwa mujibu wa mila za Kimasai, mabaki ya miili ya watoto hao waliouawa na fisi, yalizikwa Jumapili mchana katika eneo hilo.
Walioshuhudia tukio hilo walisema kwa nyakati kuwa ilikuwa saa 5:00 usiku, siku ya Jumamosi ya Machi 4, mwaka huu wakati fisi walipovamia nyumba hiyo inayomilikiwa na Ngaruma Parisuloi (38) katika kijiji cha Olojomenoku, Kata ya Nainokanoka, na kwenda hadi kwenye chumba walicholala watoto.
Mama yao Naitopi Ngaruma, ndiye alikuwa mtu wa kwanza kufika eneo la tukio na kukuta fisi mmoja akiwa tayari amepasua vichwa vya watoto wake na ubongo kutapakaa kitandani na sakafuni, huku mnyama huyo akiendelea kuitafuna miili yao.
Mama huyo alipiga kelele zilizomleta baba wa Boma, Ngaruma Parisuloi ambaye hadi kufika chumbani humo tayari fisi alikuwa amewaacha watoto na kuanza kumshambulia mkewe. Mnyama huyo alikuwa amemkaba yule mama shingoni akiwa amemuumiza vibaya.
Ngaruma ikabidi aanze kumshambulia fisi katika jitihada za kumnusuru mkewe lakini mnyama huyo alimvamia pia. Baba huyo naye aling’atwa mkono na kujeruhiwa vibaya, kabla majirani hawajafika kutoa msaada.
Fisi huyo aliuawa baada ya kukurupushwa kutoka ndani na kukimbilia zizini ambako pia aliishambulia mifugo na kuua ndama mmoja, mbuzi na kondoo kabla ya kuzidiwa nguvu na watu waliokusanyika bomani hapo kumshambulia.
Fisi hao pia wanadaiwa kuwajeruhi watu wengine kadhaa, wanne kati yao vibaya na ambao kwa sasa wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Karatu huku mipango ikiendelea ili wahamishiwe jijini Arusha kwa matibabu zaidi.