Kiungo wa Manchester United, Marouane Fellaini huenda akaihama klabu hiyo kabla ya dirisha la usajili halijafungwa usiku wa kuamkia kesho.
Klabu ya Fenerbahce Uturuki imetajwa kuwa mstari wa mbele kumuwania Fellaini ambaye alisajiliwa na Man Utd mwaka 2013 akitokea Everton kwa ada ya Pauni milioni 27.5.
Fellaini yu njiani kuondoka Old Trafford, kufuatia ugumu wa upatikanaji wa nafasi katika kikosi cha kwanza cha meneja Jose Mourinho, ambacho kwa sasa kina wachezaji wengi wanaocheza nafasi ya kiungo.
Tangu msimu wa 2017/18 ulipoanza mapema mwezi huu, kiungo huyo kutoka nchini Ubelgiji, amebahatika kucheza mchezo mmoja dhidi ya Leicester City mwishoni mwa juma lililopita, hali ambayo inatishia uwezekano wa kucheza mara kwa mara kama ilivyokua misimu miwili iliyopita.
Mbali na Fenerbahce, mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC nao wapo kwenye orodha ya kuhitajo huduma ya Fellaini mwenye umri wa miaka 29.
Wakati huo huo Man Utd hawatofanya usajili wa mchezaji yoyote ndani ya saa kadhaa kabla ya dirisha halijafungwa, na hii ni kwa mujibu wa mwandishi wa habari Duncan Castles.