Mamalaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Nchini (EWURA) imetangaza bei mpya elekezi za mafuta zitakazoanza kutumika maeneo yote nchini kuanzia leo.
Katika bei hizo mpya zilizotolewa jana na Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa EWURA, Titus Kaguo alisema kuwa kunaongezeko la bei katika mafuta ya petroli na dizeli huku mafuta ya taa yakishuka bei.
Ongezeko hilo la bei linatokana na sababu ya mabadiliko ya bei ya mafuta katika soko la dunia sambamba na kuimarika kwa thamani ya dola ya Marekani dhidi ya shilingi ya Tanzania.
Kwa upande wa mafuta ya dizeli yameongezeka Tsh 43 kwa lita huku mafuta ya petroli yakiongezeka Tsh 25 katika kila lita moja.
Afisa huyo alisema kuwa, bei hizo mpya haziwahusu wateja kutoka mkoa wa Tanga ambao wao wataendelea kutumia bei za mwezi uliopita kutokana na mkoa huo kuwa na bandari inayotumika kushushia na miundombinu ya kuhifadhi mafuta kiasi cha kuwa na akiba kubwa ya mafuta yaliyoingia nchini mwezi uliopita.