Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekataa kusaidia kuutatua mgogoro wa jimbo la Catalonia wakisema ni wajibu wa serikali ya Hispania na Barcelona kutafuta suluhu ya msuguano huo wa kisiasa.
Hayo yamesemwa na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk wakati wa kilele cha mkutano wa viongozi wa Umoja huo uliofanyika jijini Brussels nchini Ubelgiji ambapo amesema kuwa suala la kutaka kujitenga kwa Catalonia haliko katika ajenda za mkutano huo.
Amesema ” Sisi sote tuna mawazo yetu, hisia na tathimini zetu lakini kwa taarifa tu hakuna nafasi ya Umoja wa Ulaya kuingilia mgogoro huo na nchi wanachama wanaelewa fika kuwa hakuna nafasi hiyo”.
Hayo yamejiri mara baada ya Rais wa Jimbo la Catalonia, Carles Puigdemont kupuuza muda wa mwisho aliopewa na serikali ya Hispania wa kubatilisha nia yake ya kutaka kutangaza uhuru wa jimbo hilo ambapo siku tatu alizopewa kufanya hivyo zimemalizika.
Hata hivyo, pamoja na kumalizika kwa muda wa siku tatu aliopewa, Puigdemont amemuandikia barua waziri mkuu wa Hispania, Mariano Rajoy akimtishia kutangaza uhuru wa jimbo la Catalonia.