Mchekeshaji maarufu Bongo, Ebitoke amesema kuwa Idris Sultan ndiye msanii ambaye anautangaza zaidi utalii na nchi kupitia umaarufu wake ulioupata kwenye sanaa tofauti na wasanii wengine wote.
Idris ambaye alipata kujulikana zaidi baada ya kushinda Big Brother Africa 2014, Oktoba 2020 aliweka rekodi ya kuwa staa wa nne nchini kufika kileleni mwa Mlima Kilimanjaro (Uhuru Peak) baada ya Lady Jaydee, MwanaFA na Dude.
Ebitoke amesema Idris amekuwa akijitahidi kutembelea vivutio vya utali nchini na kutumia vizuri mitandao yake ya kijamii kuonesha mazuri aliyokutana nayo huko.
“Naweza kusema tunazidiwa na wasanii wa nje, hawa wanaweza kutoka kwao na kuja hapa kutangaza utalii, lakini sisi hapa tumejiweka kama kimaonesho sana, msanii akionekana Ngorongoro au Zanzibar anaonekana kama anakula bata tu,” anasema Ebitoke na kuongeza;
“Mfano wetu ni Idris Sultan, akisafiri unaona kabisa huyu mtu anatangaza utalii, ana mchango mkubwa katika kuutangaza utalii kulingana na maudhui yake mtandaoni akisafiri. Licha ya hivyo tumeona pia anashiriki kwenye filamu kubwa za kimataifa, huko ni kuitangaza nchini pamoja na utalii.”
Utakumbuka Machi 26, mwaka huu Idris alikuwa Mtanzania wa kwanza kuonekana katika mtandao mkubwa wa kuonesha filamu duniani, Netflix wenye watumiaji zaidi ya milioni 200 kupitia Filamu ya Slay iliyokutanisha na mastaa wa Afrika kama Ramsey Nouah, Fabian Adeoye Lojede, Simphiwe Ngema, Amanda Du-Pont na wengineo.