Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte amekiri kwa kusema kwamba aliwahi kuua washukiwa wa uhalifu mwenyewe alipokuwa meya wa Davao nchini humo.
Duterte alikuwa meya wa mji wa Davao kusini mwa Ufilipino kwa miaka 20 ambapo alijizolea sifa kwa kupunguza visa vya uhalifu.
Duterte alikuwa akihutubu katika mkutano wa viongozi wa kibiashara Ufilipino mnamo Jumatatu kabla ya kufunga safari kuelekea ng’ambo.
Matamshi hayo yanakaribiana na matamshi aliyoyatoa mwaka 2015, alipokiri kuua wanaume watatu walioshukiwa kutekeleza makosa ya utekaji nyara na ubakaji mjini Davao.
Lakini saa chache kabla ya kusema hayo, alikuwa amesisitiza kwamba “Mimi si muuaji”, alipokuwa akitoa hotuba wakati wa tuzo ya mtu aliyefanya vyema zaidi Ufilipino.
Karibu watu 6,000 wanadaiwa kuuawa na polisi na magenge ya watu wenye silaha tangu Duterte aanzishe vita dhidi ya mihadarati baada ya kuchaguliwa mwezi Mei.