Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba amesema kuwa Tanzania ina chakula cha kutosha na haina njaa.
Waziri huyo amesema kuwa watu wanaoneza taarifa za kuwepo kwa njaa Tanzania wana lengo la kuingiza mahindi yao yasiyo na ubora ili wafanye biashara jambo ambalo serikali imelikataa.
Pia Dkt Tizeba amesema kilichotokea ni kupanda kwa bei ya mahindi, hali iliyosababishwa na uamuzi wa serikali kuuza nafaka hiyo katika mataifa jirani yaliyokuwa na uhitaji mkubwa, ingawa kiwango kilichouzwa kilikuwa ni sehemu ya mahindi ya ziada.
Amesema kupanda bei kwa mahindi kulitarajiwa na ni kwa kawaida na wala hakuwezi kumaanisha kuwa Tanzania kuna njaa wakati nafaka zote zinapatikana kila kona ya Tanzania
Amewasihi wananchi waache tamaduni ya kung’ang’ania chakula cha aina moja na kuwataka kutumia mchele na viazi kama wanaona mahindi yamepanda bei.
Waziri huyo amepiga marufuku mtu yoyote kutoa taarifa za njaa kwa kuwa serikali ndiyo inayojua hali ya chakula kupitia vyanzo vyake.