Aliyekuwa katibu mkuu wa Chama Cha Democrasia na Maendeleo (Chadema) Wilbroad Slaa amekanusha taarifa za kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).
Akizungumza kwa njia ya simu, Dk Slaa alisema taarifa hizo si sahihi kwani alishaahidi kwamba hatarudi kwenye siasa za vyama.
Amesema hawezi kuyumba kwenye uamuzi wake licha ya kukataa kuweka wazi kwamba ni lini atarejeea nchini, alisisitiza kuwa msimamo wake wa kuachana na siasa za vyama uko palepale.
“Maneno yangu hayayumbi, sitafanya siasa za vyama, nimeachana nazo. Naomba msiniingize kwenye siasa uchwara, sizifanyi hizo… Saisa ni ajenda. Hizo siasa za kishabiki zifanyeni nyinyi huko Tanzania, mimi sifanyi ushabiki, hakuna mtu anayekula ushabiki, ndiyo maana siasa zangu siku zote ni ajenda, Watu wanataka maji, wanataka chakula, wanataka elimu bora, si ushabiki”
“Kwa miaka 20 niliyokuwa kwenye siasa sijawahi kufanya ushabiki, nilitafuta ajenda na kuipanga mikakati kwa ajili ya wananchi” alisema Dk Slaa alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.
Amesema atasimama kupiga kelele kwa ajili ya Tanzania pale atakapoona mambo yanakwenda kombo na atafanya hivyo kwa mustakabali wa Taifa si siasa.
Septemba 25, 2015 akizungumza na wandishi wa habari kwa zaidi ya saa 2 kisha kutangaza kujitoa Chadema, alisema ni afadhali apotee kwenye ulimwengu wa siasa duniani kuliko kumuunga mkono Lowassa.
Source: Tanzania Daima