Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lengo lake mwaka huu ni kuhakikisha wanaimarisha sekta ya viwanda ili kupunguza uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Hayo ameseyasema jana wakati wa hotuba yake kwenye sherehe ya mahadhimisho ya miaka 53 ya mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika uwanja wa Aman visiwani humo ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Dk Shein amesema sekta ya viwanda imechangia pato la taifa kwa asilimia 19.8 mwaka 2015 kutoka asilimia 16.8 mwaka 2014, hivyo kuboreshwa kwa sekta hiyo kutaisaidia Zanzibar kuwa na uwezo wa kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi.
Amesema viwanda vitatu vinayomilikiwa na watu binafsi, vimeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wake, ambavyo ni kiwanda cha Maziwa kinachomilikiwa na mfanyabiashara maarufu Salim Said Bahressa, Kiwanda cha Milk Co-operation na kiwanda cha kusaga unga na makonyo.
Dk Shein amesema kiwanda cha karafuu cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kinaendelea na uzalishaji wake pamoja na kiwanda cha matrekta kilichopo Mbweni, nacho kinaendelea na uzalishaji na matengenezo ya matrekta kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo ambayo imepewa kipaumbele.
Pia amesema katika uzalishaji wa mazao ya baharini, Serikali ipo katika mikakati ya kulipatia ufumbuzi soko la mwani, ambapo uzalishaji wake umeshuka kiasi cha kuwavunja moyo wakulima. Alisema Zanzibar ni nchi ya tatu ya uzalishaji wa mwani katika bara la Afrika kwa Kusafirisha mwani jumla ya tani 11,210 zenye thamani ya Sh bilioni 4.7.