Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni watu wote wanaoishi ndani ya visiwa hivyo.

 Dk Shein amesema hayo jana alipokuwa akizungumzia Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo alisema ndiyo yaliwafanya wananchi wa Zanzibar wajikomboe na waweze kujitawala wenyewe.

Katika maelezo yake Dk Shein amewataka wananchi kutambua kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni ya watu wote na kushangazwa na wale wote wanaofikiria kuwa kuna watu wataweza kuiingilia Zanzibar katika mambo yake.

Dk Shein amesema kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yana faida kubwa na malengo kwa wananchi wote wa Zanzibar kwani miongoni mwa malengo yake makubwa ni kuleta umoja, mshikamano na maendeleo bila ya ubaguzi huku akieleza azma na mafanikio ya Muungano halali wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, Dk Shein alieleza juhudi za Serikali zinazochukuliwa katika kuwaletea maendeleo wananchi kama yalivyo malengo ya Mapinduzi huku akishangazwa na baadhi ya wananchi wa Wete wanaoambiwa wasishiriki shughuli za Serikali na wao wakakubali.

Dk Shein amesema kuwa Wete imebadilika na sivyo ilivyokuwa hapo mwanzo ambapo hivi sasa huduma zote muhimu zinapatikana na zimeimarika kwani Mapinduzi yameweza kuondosha maendeleo yaliyovizwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *