Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangala amezindua kifaa kipya cha kugundua ugonjwa wa selimundu ambacho kinatoa majibu ndani ya dakika tano.

Naibu waziri huyo amesema kuwa kifaa hicho kina uwezo wa kufanya kazi kwenye mazingira yasiyo na umeme na kwamba kitaweza kutumika katika vituo vya afya ili kuwagundua wagonjwa hao mapema.

Dk Kigwangalla amesema kifaa hicho kitaboresha huduma za uchunguzi na matibabu kwa tatizo la selimundu na kuongeza uelewa kwa jamii juu ya tatizo hilo. Alisema kifaa hicho kinaweza kugundua aina mbalimbali za selimundu kwa wagonjwa kwa teknolojia rahisi isiyohitaji matumizi ya umeme wala wataalamu waliobobea.

Amefafanua kuwa kifaa hicho kimepata usajili baada ya kupitia hatua za usajili nchini ikiwemo kusajiliwa na bodi ya maabara binafsi za afya.

Amesema kuwa kitendo cha Kampuni ya Medomix cha kuagiza kitendanishi cha kupima selimundu imekuja kwa wakati sahihi ambapo nchi imekuwa na wagonjwa wengi wanaopatiwa matibabu nje ya vituo vya afya na hivyo kufanya gharama kuwa kubwa.

Kwa mujibu wa Dk Kigwangala, serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi; mikakati hiyo ni pamoja na kutengeneza mpango mkakati wa kitaifa wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo selimundu.

Pia amesema wanatoa elimu ya umma juu ya tatizo hilo, kutoa huduma za upimaji na ugunduzi wa seli mundu, upimaji wa matatizo yanayoambatana nayo na upimaji wa selimundu kwa watoto wachanga wanaozaliwa ili kuwatambua mapema pamoja na kutoa huduma za tiba na kinga kutolea huduma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *