Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye amemkabidhi bendera ya Taifa, mwanamuziki Diamond Platnumz anayekwenda kutumbuiza kwenye uzinduzi wa michuano ya Afrika (AFCON) itakayofanyika nchini Gabon kuanzia Januari 14 mwaka huu.
Akimkabidhi bendera hiyo, Waziri Nape amesema kuwa mwanamuziki huyo anakwenda kuiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo kutokana na show yake atakayoifanya nchini humo baada ya kupata mwaliko huo.
Pia Waziri Nape amemtaka Diamond Platnumz kufanya show kwa kujituma kwani kufanya hivyo ataitangaza Tanzania kupitia muziki licha la timu ya taifa kukosa nafasi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Kwa upande wake Diamond Platnumz amesema kuwa anashukuru mungu kupata nafasi ya kutumbuiza kwenye michuano hiyo kutokana na kuangaliwa na watu wengi barani Afrika pamoja na dunia kwa ujumla.
Mkali huyo kutoka WCB ameongeza kwa kusema kuwa anaishukuru Serikali kutambua mchango wake wa sanaa mpaka kumkabidhi bendera ya taifa kwa ajili ya kwenda kuiwakilisha nchi kupitia michuano hiyo.
Ikumbukwe kuwa mkali huyo alitoa burudani kwenye sherehe ya utoaji tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika zilizofanyika jijini Abuja nchini Nigeria wiki iliyopita.