Wasanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’na Faustina Charles ‘Nandy’ leo wamewasili katika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) baada ya kusambaza picha za utupu mtandaoni.
Wasanii hao wanaitikia wito wa TCRA ikiwa ni siku chache baada ya kusambaa kwa video zao zinazokiuka maadili.
Nandy aliwasili TCRA saa 5:48 asubuhi leo Aprili 19 na Diamond aliwasili saa 6:15 mchana. Diamond alisindikizwa na menejimenti yake ikiongozwa na Said Fella.
Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Sanaa na Utamaduni, Dk Harrison Mwakyembe alizungumza bungeni kuwa wasanii hao walikamatwa na kuhojiwa kuhusu kusambaa kwa video zinazokiuka maadili.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alithibitisha kuwahoji wasanii hao.