Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi amekifunga Chuo cha Ualimu cha Nkuruma kilichopo Mkoka na kuagiza uongozi wa chuo kurudisha fedha zote za ada walizolipa wanafunzi ili ziwasaidie kulipia vyuo vingine.

Ametoa agizo hilo wakati wa mkutano na wanafunzi pamoja na uongozi wa chuo hicho kuhusu kutafuta suluhu ya mgogoro ambao ulianza Septemba 16, mwaka huu.

Ndejembi amefikia hatua ya kukifunga chuo kutokana na wanafunzi kugoma kufanya mitihani ya chuo ya kumaliza mwaka wa masomo kwa madai chuo hakitambuliwi na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Amesema kukifungia chuo pekee haitoshi wanatakiwa kurudisha fedha zote za ada walizolipwa na wanafunzi katika mwaka huo wa masomo uliopita ili kuwasaidia kulipa vyuo vingine.

Amewataja wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kuwa ni mmiliki wa chuo, Mathew Nkurlu, Msajili wa Chuo, Yohana Michael, Mhasibu Elieth Ruben, wakufunzi Pendael Petro na Christopher Mabatian.

Ndejembi alitaja sababu za kuagiza wakamatwe viongozi hao wa chuo ni kuwa walihusika kushiriki katika kufanya udanganyifu na kuwatapeli wanafunzi hao huku wakijua kinachoendelea.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *