Tajiri kutoka Nigeria Aliko Dangote ndiye mtu mweusi aliye tajiri zaidi duniani kwa mujibu wa jarida la Forbes.
Kati ya watu 2,043 ambao wameorodheshwa kuwa mabilionea duniani katika orodha ya Forbes yam waka huu, ni watu 10 pekee ambao ni weusi.
Dangote amehifadhi taji la kuwa mtu mweusi tajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa takriban $14.1 bilioni.
Anafuatiwa na Mnigeria mwenzake Mike Adenuga ambaye utajiri wake unakadiriwa kuwa $5.3 bilioni.
Tajiri anayejihusisha na ujenzi ambaye ana uraia wa Saudi Arabia na Ethiopia Mohammed Al-Amoudi ambaye alikuwa na utajiri wa $8.4 bilioni aliondolewa kwenye orodha hiyo mwaka huu baada ya Forbes kuamua kuwaondoa mabilionea kutoka Saudi Arabia kwenye orodha yam waka huu.
Raia wa Zimbabwe aliyewekeza katika sekta ya mawasiliano, na ambaye hutoa pesa nyingi kwa hisani, Strive Masiyiwa, amejiunga na orodha ya watu weusi walio mabilionea.
Binti wa aliyekuwa rais wa Angola, Isabel dos Santos, Mmarekani anayejihusisha na vyombo vya habari Oprah Winfrey na tajiri wa mafuta kutoka Nigeria Folorunsho Alakija bado ndio wanawake pekee weusi kwenye orodha ya mabilionea duniani, kwa mujibu wa jarida hilo.
Marekani ndiyo nchi iliyo na mabilionea wengi duniani, ambapo ina mabilionea 585, ikifuatwa na China. Jimbo la California pekee lina mabilionea 144, zaidi kushinda mataifa yote isipokuwa Marekani na China.