China imeionya Marekani kuwa haiogopi vita vya kibiashara wakati huu ikitishia kutoza kodi ya zaidi ya dola bilioni 3 kwa bidhaa kutoka nchini Marekani katika kile kinachoonekana kujibu tangazo la rais Donald Trump kutoza kodi dhidi ya bidhaa kutoka China.
Utawala wa Beijing umetoa orodha ya bidhaa ambazo zitalengwa na kuongezewa ushuru wa hadi kufikia asilimia 25 kuanzia kwenye matunda hadi kwa nyama ya nguruwe licha ya kuwa imeshindwa kuchukua hatua zaidi na kuonesha nia ya kuwa na mazungumzo.
Hatua za hivi karibuni zimeshuhudia masoko ya hisa yakiporomoka wakati huu Marekani, ambayo inaituhumu Uchina kwa wizi wa haki miliki pamoja na hatua nyingine ambazo sio za haki dhidi ya makampuni yake, huenda ikachochea vita ya kibiashara.
Mapema rais Donald Trump alitia saini amri ambayo itaweka ukomo kwa uwekezaji wa makampuni ya Uchina nchini humo.
Hatua ya Trump haijachukua mara moja hatua za kuweka ushuru mpya, lakini ndani ya majuma mawili waziri wa biashara wa Marekani anatarajiwa kutangaza bidhaa zilizolengwa kwenye amri hiyo ya rais Trump.
Wakati huu rais Trump akionekana kutafuta ugomvi na mataifa yenye nguvu, utawala wa Beijing umeonya kuwa vita vya kibiashara havitamnufaisha yeyote na haitakaa kimya kuona Marekani ikitoa adhabu kwa biashara zake.
Waziri wa viwanda Wilbur Ross alisema Alhamisi ya wiki hii kuwa hatua za kulinda haki zake miliki ililenga kuifanya China ije kwenye meza ya mazungumzo na kujadiliana kutafuta njia za kudhibiti wizi huo.