Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (CHAKUA) kimeiomba serikali kuhakikisha matumizi ya tiketi za elektroniki katika sekta ya usafirishaji nchini yanakuwa ya lazima.
Ofisa Msimamizi wa chama hicho anayesimamia Mkoa wa Dar es Salaam, Mark Serra amesema Chakua imekuwa ikifuatilia kwa karibu mfumo huu na kubaini una manufaa makubwa kwa abiria, ambapo watatozwa nauli halali iliyoidhinishwa na Sumatra, ambazo ndizo bei elekezi kwa mujibu wa sheria.
Amesema kwa kutumia tiketi za kielekroniki, itawalazimu wamiliki wa vyombo vya usafiri kutokupandisha nauli katika kipindi cha mvua au jua kali, kipindi cha wanafunzi wapotoka vyuoni au mashuleni pamoja na kipindi cha sikukuu au mwanzoni mwa mwaka, ambapo mabasi mengi huita vipindi hivyo ni vya kuvuna abiria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Hassan Mchanjama alisema kutumika kwa mfumo huo, utawanufaisha abiria na kuokoa muda wa kwenda kwenye vituo vya mabasi kwa ajili ya kukata tiketi badala yake mfumo huu utamuwezesha abiria kukata tiketi akiwa nyumbani, ofisini au sehemu yoyote kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Amesema mfumo huo pia utarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za abiria pindi inapotokea ajali kujua abiria wangapi wamepoteza maisha, waliopata ulemavu pamoja na waliopoteza mali zao, ambapo kwa mfumo unaotumika sasa hivi ni vigumu kupata takwimu na taarifa sahihi za abiria.
Source: Habari Leo