Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imeteua majina sita ya wagombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene imesema kuwa wateule hao watakamilisha hatua zingine za uteuzi kwa mujibu wa utaratibu, Kanuni za Bunge na Uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki.
Pia taarifa hiyo imewataja wagombea hao kuwa ni Profesa Abdalla Safari, Salum Mwalimu, Ezekiel Wenje, Josephine Lemoyan, Lawrence Masha na Pamela Massay.
Katika majina hayo sita yaliyoteuliwa na kamati hiyo ni majina ya watu wawili tu ndiyo yatakayopita kwa ajili ya kuiwakilisha Chadema kwenye bunge hilo la Afrika Mashariki (EALA).
Hapo awali Chadema ilipeleka majina ya watu wawili tu ambao ni Ezekiel Wenje pamoja na Lawrence Masha ambapo walipigiwa kura za hapana bungeni kutokana na Chadema kukiuka taratibu za kuteua wagombea.