Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Vincent Mashinji amesema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limevunja katiba ya nchi Ibara ya 137.
Amesema hayo leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za Chama hicho jijini Dar es Salaam.
Mashinji amesema kuwa Bunge kuomba fedha za ziada nje ya bajeti iliyoidhinishwa na bunge bila kupitisha maombi hayo bungeni kama katiba inavyotaka.
Amesema kuwa ‘’Kwa mujibu wa sheria ya uendeshaji wa bunge ya mwaka 2008 Kifungu cha 31 kinaeleza kuwa fedha zote kwa ajili ya uendeshaji wa bunge zinawekwa kwenye mfuko maalum kama ulivyoanzishwa na sheria hiyo na msimamizi mkuu wa fedha hizo ni Katibu Mkuu wa Bunge kwa mujibu wa kupengele cha (2) na (3)cha katiba.
“Kati ya Juni 21, 2017 na Agosti 15, 2017 Katibu wa Bunge aliandika barua tatu tofauti akiomba fedha zaidi ya shilingi bilioni tisa (9,966,464,000.00) kwa Waziri wa Fedha na kwa Katibu Mkuu wa Hazina kwa ajili ya kugharamia bajeti ya ziada na fedha za matumizi mengineyo kwa ajili ya bunge ikiwa nje ya bajeti iliyokuwa imeidhinishwa na bunge na kuwekwa katika mfuko maalum wa bunge katika mwaka wa fedha wa 2016/17.
Pia amesema kuwa “Tangu wakati huo mpaka Agosti 15 mwaka huu serikali ilishatoa bajeti ya ziada kwa bunge kiasi cha shilingi bilioni 7 kutoka katika mfuko mkuu wa hazina bila kufuata masharti ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”