Mfanyabiashara  Harbinder  Singh Sethi na James  Rugemalira wamepandishwa kizimbani kwa mara nyingine katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 12, badala ya mashtaka sita waliyosomewa awali.

Miongoni mwa mashtaka hayo 12 ya  uhujumu uchumi yamo mashtaka matano ya kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158. 27.

Akiwasomea hati mpya ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shedrack Kimaro kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alidai wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kighushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia Serikali hasara na kutakatisha fedha.

Washtakiwa hao katika shtaka la kwanza wanadaiwa, Rugemarila ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP wanadaiwa kuwa   kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jiji Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kimaro alidai katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, 2011na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma na watumishi wa umma  walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Kwa upande shtaka la tatu, Sethi  anadaiwa  kuwa   Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni  na kuonyesha yeye ni mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.

Seth katika shtaka la nne anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14a ya usajili wa kampuni kwa ofisa msajili wa kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonyesha kwamba yeye ni mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka la tano, washtakiwa wote, wanadaiwa kuwa kati ya  Novemba 28/29, 2011 na Januari 23, 2014 makao makuu Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi Tawi St Joseph kwa ulaghai washtakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), walijipatia USD 22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27.

Katika shtaka sita la kusababisha hasara,  washtakiwa hao wanadaiwa kuwa   Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  kati Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya USD 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *