Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya simu za mkononi ya Halotel, Do Hong (44) na wenzake saba wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 10 likiwamo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 459.

Hong ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Viettel, alifikishwa mahakamani hapo jana pamoja na washitakiwa Dilshad Ahmed (36), Rohail Yaqoob(47), Khalid Mahmood (59), Ashfaq Ahmad (38), Muhamad Aneess(48), Imtiaz Ammar (33) wote raia wa Pakistan na Ramesh Kandasamy (36) raia wa Sri-Lanka wanaokabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.

Wakili wa Serikali, Jehovanes Zacharia alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa washitakiwa Ahmed, Yaqoob, Mahamood, Ahmad, Anees, Kandasamy na Qammar, Novemba mwaka jana Dar es Salaam walikula njama kutenda kosa la kutumia vifaa vya mitandao.

Alidai kati ya Novemba mwaka jana na Februari mwaka huu, jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao walitengeneza mfumo wa kutumia huduma za mtandao ili kukwepa kodi ya kupokea na kusambaza simu za kimataifa bila kibali cha TCRA.

Zacharia alidai washitakiwa katika kipindi hicho waliendesha hiyo mifumo ya kupokea na kusambaza simu za kimataifa bila ya kuwa na leseni. Alidai Novemba 20, mwaka jana, washitakiwa hao waliingiza vifaa vya kielektroniki bila ya kuwa na leseni na kwamba katika tarehe isiyofahamika Novemba mwaka huohuo walisimika vifaa hivyo ikiwamo sim box yenye namba ya siri 1152000.8.n.t.n na Laptop mbili aina ya Dell bila ya kuwa na kibali cha TCRA.

Katika kipindi hicho, washtakiwa hao wanadaiwa kuunganisha vifaa hivyo na huduma za mitandao ili kupokea na kusambaza mawasiliano bila ya kuthibitishwa na TCRA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *