Ngege mpya za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Q400 zinatarajia kuanza kutoa huduma za usafiri nchini Kenya kuanzia mwakani.

Hayo yalibainika jana wakati wa Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Kenya uliofanyika Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali.

Akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Aziz Mlima alisema kati ya masuala watakayojadiliana ni kuanzia mwakani ndege hizo za ATCL kuanza kutoa huduma nchini Kenya.

Alisema kwa kuwa ndege za Kenya zinatoa huduma nchini, hivyo watajadiliana kuhakikisha huduma hiyo na nyingine zinafanyika kwa ushirikiano baina ya nchi hizo kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.

Ndege hizo za ATCL zilianza safari zake Oktoba 14, mwaka huu na zinatoa huduma katika viwanja vya Mwanza, Zanzibar, Arusha na Kigoma kwa safari za ndani na Moroni, Comoro kwa safari za nje. Lakini mwezi huu wanatarajia kupanua huduma nchini na nchi jirani kwa kuongeza safari za Kilimanjaro, Mtwara, Dodoma na Tabora.

Akizungumzia mkutano huo, Dk Mlima alisema kwa mara ya mwisho mkutano kama huo ulifanyika mwaka 2012, hivyo kikao hicho kitajadili utekelezaji ya maazimio waliyofikia kwa wakati huo na changamoto zake ili kuweza kupata ufumbuzi.

Alisema mkutano huo utatoa nafasi kwa wajumbe kujadiliana kisekta ili kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano na njia zitakazowezesha kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.

Naye kiongozi wa timu kutoka Kenya, Balozi Ben Ogutu alisema mkutano huo utatoa fursa ya kujadiliana katika sekta zote kutokana na historia ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ulioanza tangu wakati wa uhuru.

Alisema wajumbe watangalia masuala mapya ya ushirikiano kwa kuangalia ule wa awali kulingana na mazungumzo ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais John Magufuli walipokutana hivi karibuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *