Nguli wa mashindano ya riadha kutoka nchini Jamaica, Usain Bolt ameweka wazi kuwa ‘hana nia ya kurudi tena kwenye riadha’.
Bolt ameweka wazi msimamo huo baada ya kuhojiwa na waandishi wa habari waliotaka kufahamu iwapo amebadili mawazo yake kufuatia kupokonywa medali moja ya dhahabu aliyoshinda mwaka 2008.
‘Nilimuuliza Michael Johnson (mkimbiaji wa zamani wa Marekani), kwanini ulistaafu wakati uko kwenye kilele cha ubora wako? Akanijibu; Nimeshafanya yote niliyotaka kufanya kwenye riadha kwahiyo sina sababu ya kuendelea kubaki’
Amekaririwa Bolt akifafanua sababu ya kufikia uamuzi wa kustaafu.
Bolt ambaye ameshinda tuzo ya Laureus Sportsman of the Year nchini Ufaransa alipokuwa akichuana na Mo Farah na Andy Murray amedai kuwa amefanikiwa kutimiza ndoto na malengo aliyoyaweka kwenye riadha hivyo hana sababu ya kuendelea kushindana.
Kwa kipindi chote alichokuwa mkimbiaji Bolt amefanikiw akukusanya jumla ya medali 8 za dhahabu za mashindano ya Olimpiki huku medali moja akipokonywa kutokana na kosa alilolifanya mkimbiaji mwenzake Nesta Carter.
Bolt amefanikiwa kutwaa medali za dhahabu kwa mara tatu katika vipindi mbalimbali vya mashindano ya olompiki kwa mbio za
100m, 200m na 4x100m.