Mwanariadha, Usain Bolt ameshindwa kumaliza mbio zake za mwisho za ubingwa wa dunia jijini London baada ya kuumia misuli wakati wa mbio hizo.
Bolt alipata mkakamao wa misuli na kulazimika kuondoka uwanjani alipokuwa akikimbia mbio za kupokezana vijiti za 4x100m ambazo timu ya Uingereza ilishinda.
Mwanariadha mwenzake, Yohan Blake amesema kuwa mbio zilicheleweshwa dakika 10, wakisubiri kwa dakika 40 ndiyo chanzo cha Bolt kuumia misuli.
Bolt alikuwa ametumai kwamba angemaliza maisha yake ya ukimbiaji kwa kushinda dhahabu mbili mashindano hayo ya London lakini ameondoka sasa na nishani ya shaba pekee aliyoishinda kwenye mbio za mita 100 wikendi iliyopita.
Sekunde chache baada yake kupokezwa kijiti awamu ya mwisho ya mbio hizo, alitatizima na kuanguka sakafuni.
Daktari wa timu ya Jamaica Kevin Jones amethibitisha kwamba Bolt alipatwa na mkakamao wa misuli ya mguu wake wa kushoto.
Bingwa wa mbio za 110m za kuruka viunzi Omar McLeod, aliyeongoza timu ya Jamaica ambayo ilikuwa imeshinda ubingwa wa mbio za 4x100m katika makala manne yaliyopita ya ubingwa wa dunia, alikubaliana na mtazamo wa Blake.
Mshindi wa mbio za 100m Justin Gatlin alisema Bolt ‘ndiye bado bora zaidi duniani’ baada yake kushinda nishani ya fedha na timu yake ya Marekani.