Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imewapa siku 30 kuanzia Novemba 14, mwaka huu wadaiwa wake sugu 154,000 kurejesha fedha wanazodaiwa.
Vinginevyo, imesema watakamatwa na kulazimishwa kulipa madeni na gharama za kuwasaka.
Kwa mujibu wa bodi hiyo, wadaiwa wote wanaoangukia katika mkumbo huo, watatangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari Novemba 13, siku moja kabla ya kuanza kwa notisi hiyo ya siku 30, isipokuwa kwa wale ambao watakuwa tayari wamelipa.
Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul Razaq Badru alisema wadaiwa hao ni wa kuanzia mwaka 1994 mpaka sasa ambao madeni yao yameiva.
Alisema hadi sasa serikali inadai Sh trilioni 2.6 kutoka kwa wadaiwa hao ambao walikopeshwa kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu lakini hawajarejesha mikopo hiyo na hivyo kuleta changamoto kwa waombaji wapya.
Alisema wadaiwa hao sugu wanapaswa kukumbuka kuwa kutolipa madeni yao ni kuvunja Mkataba na Sheria ya Bodi hiyo Namba 9 ya mwaka 2004, 19 (1).
Sheria hiyo ya mwaka 2004 Kipengele cha pili kinasema mdaiwa atapewa penalti ya asilimia tano juu ya ile asilimia tano iliyokuwa ikitozwa kabla, kwa kila mwezi kwenye deni lililobakia au alilonalo. Aidha, kipengele cha tatu kinasema mdaiwa ataongezewa gharama za kumtafuta alipo ili alipe deni lililoingiwa na bodi.
Vipengele vingine kwenye sheria hiyo vinasema mdaiwa atawekwa kwenye orodha ya wadaiwa sugu ‘blacklist’ na maelezo yake yatapelekwa kitengo cha kumbukumbu ya wakopaji na hivyo kushindwa kukopa sehemu nyingine yoyote.
Pia mdaiwa atazuiliwa kupata udhamini wa serikali au udahili wa masomo ya juu kwenye vyuo vyovyote ndani na nje ya nchi. Kadhalika, maelezo yao yatapelekwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kitengo cha Uhamiaji na balozi zote ambako watakataliwa safari zozote za kwenda nje ya nchi.
Badru alisema awali selikali ilitoa mikopo hiyo kwa wanafunzi, kwa kuweka bayana kwamba fedha walizopewa ni mikopo na wala si msaada au ruzuku, hivyo zinapaswa kujereshwa mara baada ya mdaiwa kuhitimu masomo yake; au pindi atakapositisha masomo yake kwa sababu mbalimbali.