Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Abdul Razaq amesema wadaiwa sugu wa mikopo wa Elimu ya Juu watachukuliwa hatua kali iwapo hawatarejesha mikopo hiyo ndani ya mwezi mmoja tangu leo.
Hayo aliyamesema leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusiana na wanufaika waliokopeshwa na na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ambao muda wao wa kurejesha umepita.
Amesema wadaiwa hao ni wa tangu mwaka wa masomo wa 1994/95 ambao ni 93,500 na kati ya hao 81,055 wanaendelea kulipa mikopo yao na wanufaika 12,445 waliobainika na kupelekewa ankara zao hawajaanza kulipa madeni yao.
Aliongeza kuwa wengine waliobainika na kupelekewa ankara zao za madeni ni 142,470 wenye mikopo ya jumla ya Sh.239,353,750,176.27 ambayo imeiva lakini bado hawajajitokeza kulipa mikopo hiyo.
Alidai wanufaika hao wamevunja sheria kama ilivyobainishwa kwenye kifungu cha sheria namba 19 A(1) cha Sheria ya Bodi ya Mikopo.
Alizitaja baadhi ya hatua kali zilizochukuliwa na bodi hiyo kuwa ni pamoja na kutoa notisi ya siku thelathini ili walipe kiasi chote cha mikopo wanayodaiwa, kuyatangaza majina ya wadaiwa sugu hadharani kupitia tovuti (website) ili waajiri na wadhamini wao na wadau wenye taarifa za wadaiwa wawasilishe madai hayo bodi ya mokopo mara moja na kukamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani wadaiwa wote sugu ili walipe madeni yao na gharama za kuwatafuta na kuendesha kesi.
Aidha bodi imewapongeza na kuwashukuru wale wote ambao wamekwishalipa au kuendelea kulipa huku akisisitiza wadaiwa kulipa kabla hatua stahiki hazijachukuliwa.
Picha kwa hisani ya Global Publishers