Mwanamuziki wa Marekani, Beyonce ametumia maneno ya lugha ya Kiswahili katika wimbo wake Spirit ambao upo kama ‘soundtrack’ kwenye filamu ya The Lion King.
Mwanzoni kabisa mwa ngoma hiyo yenye dakika 4:37, yanasikika maneno ya Kiswahili sanifu yakisema: ‘Uishi kwa muda mrefu mfalme
(Uishi kwa uishi kwa).
Unaweza kuona ni jinsi gani lugha ya Kiswahili inakua kwa kasi na imekuwa na nafasi kubwa kwenye sanaa ulimwenguni kote kiasi cha kutokuwa ajabu tena kuisikia kwenye filamu na nyimbo za wasanii wakubwa.
Ukiacha hili la Beyonce, miaka kadhaa nyuma hata Michael Jackson kwenye Liberian Girl, Omario, Nas na wengino waliwahi kuimba Kiswahili katika ngoma zao, hivyo inatupa tafsiri kuwa tunahitaji kuwekeza zaidi kwenye lugha hii.
Inatarajiwa kusikia maneno mengi ya Kiswahili yakitumika katika filamu ya The Lion King maana ndani yake kuna mhusika mmoja anaitwa Simba, jina la Kiswahili la mnyama ila jambo la ajabu utaona aliyeingiza sauti yenye maneno ya Kiswahili kwenye wimbo, Spirit siyo Mtanzania wakati Bongo tuna wataalamu wa lugha hii tamu.
Disney wanasema wimbo huo unapatikana kwenye albamu ambayo imeandaliwa na Beyonce mwenyewe kama ‘soundtrack’ ya filamu ya The Lion King, ambayo imebeba kisa kisa cha simba mdogo anayetafuta namna ya kuwa mfalme.
Filamu hiyo imeigizwa na mastaa wengi akiwamo Beyonce, Chaldish Gambino, Seth Rogen, Chiwetel Ejiofor, Billy Eichner na Keegan Michael.